Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 91 (Sura 91)
1; Naapa kwa jua na mwangaza wake!
2; Na kwa mwezi unapo lifuatia!
3; Na kwa mchana unapo lidhihirisha!
4; Na kwa usiku unapo lifunika!
5; Na kwa mbingu na kwa aliye ijenga!
6; Na kwa ardhi na kwa aliye itandaza!
7; Na kwa nafsi na kwa aliye itengeneza!
8; Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake,
9; Hakika amefanikiwa aliye itakasa,
10; Na hakika amekhasiri aliye iviza.
11; Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao,
12; Alipo simama mwovu wao mkubwa,
13; Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake.
14; Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa.
15; Wala Yeye haogopi matokeo yake.

Pages ( 91 of 114 ): « Previous1 ... 8990 91 9293 ... 114Next »