Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 52 (Sura 52)
1; Naapa kwa mlima wa T´ur,
2; Na Kitabu kilicho andikwa
3; Katika ngozi iliyo kunjuliwa,
4; Na kwa Nyumba iliyo jengwa,
5; Na kwa dari iliyo nyanyuliwa,
6; Na kwa bahari iliyo jazwa,
7; Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
8; Hapana wa kuizuia.
9; Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,
10; Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
11; Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
12; Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
13; Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
14; (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
15; Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu?
16; Uingieni, mkistahamili au msistahamili – ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda.
17; Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
18; Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni.
19; Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda.
20; Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.
21; Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma.
22; Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda.
23; Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
24; Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
25; Wataelekeana wakiulizana.
26; Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa;
27; Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
28; Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
29; Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
30; Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
31; Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
32; Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
33; Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini!
34; Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.
35; Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji?
36; Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini.
37; Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka?
38; Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi!
39; Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana?
40; Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama?
41; Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika?
42; Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.
43; Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye.
44; Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana.
45; Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa.
46; Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
47; Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui.
48; Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama,
49; Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota.

Pages ( 52 of 114 ): « Previous1 ... 5051 52 5354 ... 114Next »