Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 87 (Sura 87)
1; Litakase jina la Mola wako Mlezi aliye juu kabisa,
2; Aliye umba, na akaweka sawa,
3; Na ambaye amekadiria na akaongoa,
4; Na aliye otesha malisho,
5; Kisha akayafanya makavu, meusi.
6; Tutakusomesha wala hutasahau,
7; Ila akipenda Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye anayajua yaliyo dhaahiri na yaliyo fichikana.
8; Na tutakusahilishia yawe mepesi.
9; Basi kumbusha, kama kukumbusha kunafaa.
10; Atakumbuka mwenye kuogopa.
11; Na atajitenga mbali nayo mpotovu,
12; Ambaye atauingia Moto mkubwa.
13; Tena humo hatakufa wala hawi hai.
14; Hakika amekwisha fanikiwa aliye jitakasa.
15; Na akakumbuka jina la Mola wake Mlezi, na akasali.
16; Lakini nyinyi mnakhiari maisha ya dunia!
17; Na Akhera ni bora na yenye kudumu zaidi.
18; Hakika haya yamo katika Vitabu vya mwanzo,
19; Vitabu vya Ibrahimu na Musa.

Pages ( 87 of 114 ): « Previous1 ... 8586 87 8889 ... 114Next »