Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 83 (Sura 83)
1; Ole wao hao wapunjao!
2; Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe.
3; Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.
4; Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa
5; Katika Siku iliyo kuu,
6; Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?
7; Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.
8; Unajua nini Sijjin?
9; Kitabu kilicho andikwa.
10; Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha!
11; Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo.
12; Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi.
13; Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale!
14; Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma.
15; Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi.
16; Kisha wataingia Motoni!
17; Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha.
18; Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I´liyyin.
19; Na nini kitakacho kujuvya nini I´liyyin?
20; Kitabu kilicho andikwa.
21; Wanakishuhudia walio karibishwa.
22; Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema.
23; Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia.
24; Utatambua katika nyuso zao mng´aro wa neema,
25; Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri,
26; Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana.
27; Na mchanganyiko wake ni Tasniim,
28; Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa.
29; Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini.
30; Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana.
31; Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi.
32; Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea.
33; Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao.
34; Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri,
35; Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia.
36; Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda?

Pages ( 83 of 114 ): « Previous1 ... 8182 83 8485 ... 114Next »