Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 36 (Sura 36)
1; Ya-Sin (Y.S.).
2; Kwa Haki ya Qur´ani yenye hikima!
3; Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
4; Juu ya Njia Iliyo Nyooka.
5; Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
6; Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
7; Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
8; Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.
9; Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.
10; Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
11; Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.
12; Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.
13; Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.
14; Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
15; Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
16; Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.
17; Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
18; Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
19; Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
20; Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
21; Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.
22; NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?
23; Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
24; Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.
25; Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
26; Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua
27; Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.
28; Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
29; Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!
30; Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
31; Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.
32; Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
33; Na Ishara hiyo kwao – ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!
34; Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake,
35; Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?
36; Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.
37; Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.
38; Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
39; Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
40; Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.
41; Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni.
42; Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.
43; Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,
44; Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
45; Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa…
46; Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.
47; Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.
48; Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
49; Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.
50; Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
51; Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.
52; Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
53; Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.
54; Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.
55; Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.
56; Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.
57; Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.
58; “Salama!” Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
59; Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!
60; Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet´ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.
61; Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
62; Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
63; Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.
64; Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
65; Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
66; Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?
67; Na tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.
68; Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?
69; Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur´ani inayo bainisha.
70; Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
71; Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
72; Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala.
73; Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?
74; Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!
75; Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa.
76; Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.
77; Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!
78; Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung´unyika?
79; Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
80; Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.
81; Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.
82; Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.
83; Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.

Pages ( 36 of 114 ): « Previous1 ... 3435 36 3738 ... 114Next »