Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 63 (Sura 63)
1; Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo.
2; Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa wakiyafanya.
3; Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote.
4; Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki?
5; Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi.
6; Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
7; Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu.
8; Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu – Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.
9; Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri.
10; Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema?
11; Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

Pages ( 63 of 114 ): « Previous1 ... 6162 63 6465 ... 114Next »