Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 56 (Sura 56)
1; Litakapo tukia hilo Tukio
2; Hapana cha kukanusha kutukia kwake.
3; Literemshalo linyanyualo,
4; Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso,
5; Na milima itapo sagwasagwa,
6; Iwe mavumbi yanayo peperushwa,
7; Na nyinyi mtakuwa namna tatu:-
8; Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani?
9; Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni?
10; Na wa mbele watakuwa mbele.
11; Hao ndio watakao karibishwa
12; Katika Bustani zenye neema.
13; Fungu kubwa katika wa mwanzo,
14; Na wachache katika wa mwisho.
15; Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa.
16; Wakiviegemea wakielekeana.
17; Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele,
18; Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.
19; Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa.
20; Na matunda wayapendayo,
21; Na nyama za ndege kama wanavyo tamani.
22; Na Mahurulaini,
23; Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa.
24; Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
25; Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi,
26; Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama.
27; Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani?
28; Katika mikunazi isiyo na miba,
29; Na migomba iliyo pangiliwa,
30; Na kivuli kilicho tanda,
31; Na maji yanayo miminika,
32; Na matunda mengi,
33; Hayatindikii wala hayakatazwi,
34; Na matandiko yaliyo nyanyuliwa.
35; Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya,
36; Na tutawafanya vijana,
37; Wanapendana na waume zao, hirimu moja.
38; Kwa ajili ya watu wa kuliani.
39; Fungu kubwa katika wa mwanzo,
40; Na fungu kubwa katika wa mwisho.
41; Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni?
42; Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka,
43; Na kivuli cha moshi mweusi,
44; Si cha kuburudisha wala kustarehesha.
45; Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.
46; Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,
47; Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa?
48; Au baba zetu wa zamani?
49; Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho
50; Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.
51; Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha,
52; Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu.
53; Na kwa mti huo mtajaza matumbo.
54; Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka.
55; Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu.
56; Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.
57; Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki?
58; Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza?
59; Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji?
60; Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi
61; Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua.
62; Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki?
63; Je! Mnaona makulima mnayo yapanda?
64; Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?
65; Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu,
66; Mkisema: Hakika sisi tumegharimika;
67; Bali sisi tumenyimwa.
68; Je! Mnayaona maji mnayo yanywa?
69; Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?
70; Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru?
71; Je! Mnauona moto mnao uwasha?
72; Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji?
73; Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani.
74; Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu.
75; Basi naapa kwa maanguko ya nyota,
76; Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!
77; Hakika hii bila ya shaka ni Qur´ani Tukufu,
78; Katika Kitabu kilicho hifadhiwa.
79; Hapana akigusaye ila walio takaswa.
80; Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
81; Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza?
82; Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha?
83; Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo,
84; Na nyinyi wakati huo mnatazama!
85; Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi.
86; Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu,
87; Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
88; Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa,
89; Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.
90; Na akiwa katika watu wa upande wa kulia,
91; Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.
92; Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu,
93; Basi karamu yake ni maji yanayo chemka,
94; Na kutiwa Motoni.
95; Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.
96; Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa.

Pages ( 56 of 114 ): « Previous1 ... 5455 56 5758 ... 114Next »