Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 26 (Sura 26)
1; T´aa Siin Miim. (T´.S.M.)
2; Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
3; Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
4; Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.
5; Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.
6; Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
7; Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
8; Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
9; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
10; Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,
11; Watu wa Firauni. Hawaogopi?
12; Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.
13; Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
14; Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.
15; Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
16; Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17; Waachilie Wana wa Israili wende nasi.
18; (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?
19; Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?
20; (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.
21; Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
22; Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
23; Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
24; Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
25; (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?
26; (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
27; (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.
28; (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
29; (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
30; Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
31; Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.
32; Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.
33; Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.
34; (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
35; Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
36; Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.
37; Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
38; Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.
39; Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?
40; Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda.
41; Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?
42; Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
43; Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.
44; Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
45; Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.
46; Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.
47; Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
48; Mola Mlezi wa Musa na Harun.
49; (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.
50; Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
51; Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.
52; Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
53; Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.
54; (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
55; Nao wanatuudhi.
56; Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
57; Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,
58; Na makhazina, na vyeo vya hishima,
59; Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
60; Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.
61; Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!
62; (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
63; Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
64; Na tukawajongeza hapo wale wengine.
65; Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.
66; Kisha tukawazamisha hao wengine.
67; Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.
68; Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
69; Na wasomee khabari za Ibrahim.
70; Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
71; Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
72; Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?
73; Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?
74; Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
75; Je! Mmewaona hawa mnao waabudu-
76; Nyinyi na baba zenu wa zamani?
77; Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
78; Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,
79; Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.
80; Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.
81; Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
82; Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.
83; Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.
84; Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.
85; Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.
86; Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
87; Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.
88; Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.
89; Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
90; Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.
91; Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
92; Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu
93; Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?
94; Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,
95; Na majeshi ya Ibilisi yote.
96; Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
97; Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,
98; Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
99; Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.
100; Basi hatuna waombezi.
101; Wala rafiki wa dhati.
102; Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.
103; Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
104; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
105; Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
106; Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?
107; Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
108; Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
109; Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
110; Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
111; Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?
112; Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?
113; Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!
114; Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.
115; Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.
116; Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.
117; Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.
118; Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.
119; Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.
120; Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia.
121; Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.
122; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
123; Kina A´d waliwakanusha Mitume.
124; Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu?
125; Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
126; Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
127; Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
128; Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
129; Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!
130; Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.
131; Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini.
132; Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.
133; Amekupeni wanyama wa kufuga na wana.
134; Na mabustani na chemchem.
135; Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.
136; Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.
137; Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.
138; Wala sisi hatutaadhibiwa.
139; Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
140; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
141; Kina Thamud waliwakanusha Mitume.
142; Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?
143; Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
144; Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini.
145; Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
146; Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?
147; Katika mabustani, na chemchem?
148; Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.
149; Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.
150; Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
151; Wala msit´ii amri za walio pindukia mipaka,
152; Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.
153; Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa.
154; Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
155; Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
156; Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.
157; Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.
158; Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
159; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
160; Watu wa Lut´i waliwakanusha Mitume.
161; Alipo waambia ndugu yao, Lut´i: Je! Hamumchimngu?
162; Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.
163; Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit´iini mimi.
164; Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
165; Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
166; Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!
167; Wakasema: Ewe Lut´i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!
168; Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.
169; Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.
170; Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,
171; Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma.
172; Kisha tukawaangamiza wale wengine.
173; Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.
174; Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
175; Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
176; Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.
177; Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?
178; Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
179; Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit´iini mimi.
180; Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
181; Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.
182; Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;
183; Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi.
184; Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.
185; Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa.
186; Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
187; Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
188; Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.
189; Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.
190; Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
191; Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
192; Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
193; Ameuteremsha Roho muaminifu,
194; Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,
195; Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
196; Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.
197; Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?
198; Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,
199; Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini.
200; Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.
201; Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.
202; Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.
203; Na watasema: Je, tutapewa muhula?
204; Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?
205; Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,
206; Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,
207; Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?
208; Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji –
209; Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.
210; Wala Mashet´ani hawakuteremka nayo,
211; Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.
212; Hakika hao wametengwa na kusikia.
213; Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.
214; Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
215; Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini.
216; Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda.
217; Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
218; Ambaye anakuona unapo simama,
219; Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.
220; Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
221; Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet´ani?
222; Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.
223; Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.
224; Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.
225; Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?
226; Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?
227; Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.

Pages ( 26 of 114 ): « Previous1 ... 2425 26 2728 ... 114Next »