Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 15 (Sura 15)
1; Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur´ani inayo bainisha.
2; HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.
3; Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.
4; Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.
5; Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa.
6; Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.
7; Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?
8; Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.
9; Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.
10; Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.
11; Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.
12; Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.
13; Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.
14; Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,
15; Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.
16; Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
17; Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye.
18; Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.
19; Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.
20; Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
21; Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.
22; Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.
23; Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi.
24; Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari.
25; Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.
26; Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
27; Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.
28; Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
29; Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia.
30; Basi Malaika wote pamoja walimsujudia,
31; Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu.
32; (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu?
33; Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura.
34; (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!
35; Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.
36; Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa.
37; (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula
38; Mpaka siku ya wakati maalumu.
39; Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,
40; Ila waja wako walio safika.
41; Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka.
42; Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.
43; Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote.
44; Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.
45; Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
46; (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani.
47; Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.
48; Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo.
49; Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
50; Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!
51; Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim.
52; Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.
53; Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.
54; Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?
55; Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa.
56; Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?
57; Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?
58; Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!
59; Isipo kuwa walio mfuata Luut´i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.
60; Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma.
61; Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut´i,
62; Alisema (Luut´i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana.
63; Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.
64; Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli.
65; Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.
66; Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.
67; Na wakaja watu wa mji ule nao furahani.
68; Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe.
69; Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.
70; Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?
71; Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.
72; Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.
73; Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.
74; Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.
75; Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi.
76; Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa.
77; Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.
78; Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu.
79; Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi.
80; Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.
81; Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza.
82; Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.
83; Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.
84; Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.
85; Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.
86; Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi.
87; Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur´ani Tukufu.
88; Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.
89; Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.
90; Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa,
91; Ambao wakaifanya Qur´ani vipande vipande.
92; Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote,
93; Kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
94; Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina.
95; Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.
96; Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua!
97; Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.
98; Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia.
99; Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini.

Pages ( 15 of 114 ): « Previous1 ... 1314 15 1617 ... 114Next »