Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 89 (Sura 89)
1; Naapa kwa alfajiri,
2; Na kwa masiku kumi,
3; Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja,
4; Na kwa usiku unapo pita,
5; Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili?
6; Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A´di?
7; Wa Iram, wenye majumba marefu?
8; Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?
9; Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni?
10; Na Firauni mwenye vigingi?
11; Ambao walifanya jeuri katika nchi?
12; Wakakithirisha humo ufisadi?
13; Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu.
14; Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.
15; Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu!
16; Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge!
17; Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima,
18; Wala hamhimizani kulisha masikini;
19; Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa,
20; Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi.
21; Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande,
22; Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu,
23; Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?
24; Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!
25; Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.
26; Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.
27; Ewe nafsi iliyo tua!
28; Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.
29; Basi ingia miongoni mwa waja wangu,
30; Na ingia katika Pepo yangu.

Pages ( 89 of 114 ): « Previous1 ... 8788 89 9091 ... 114Next »