Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 75 (Sura 75)
1; Ninaapa kwa Siku ya Kiyama!
2; Na ninaapa kwa nafsi inayo jilaumu!
3; Anadhani mtu kuwa Sisi hatutaikusanya mifupa yake?
4; Kwani! Sisi tunaweza hata kuziweka sawa sawa ncha za vidole vyake!
5; Lakini mtu anataka tu kuendelea na maasi kwa siku zilioko mbele yake.
6; Anauliza: Lini itakuwa hiyo Siku ya Kiyama?
7; Basi jicho litapo dawaa,
8; Na mwezi utapo patwa,
9; Na likakusanywa jua na mwezi,
10; Siku hiyo mtu atasema: Yako wapi makimbilio?
11; La! Hapana pa kukimbilia!
12; Siku hiyo pa kutua ni kwa Mola wako Mlezi tu.
13; Siku hiyo ataambiwa aliyo yatanguliza na aliyo yaakhirisha.
14; Bali mtu ni hoja juu ya nafsi yake.
15; Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.
16; Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka.
17; Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha.
18; Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake.
19; Kisha ni juu yetu kuubainisha.
20; Hasha! Bali nyinyi mnapenda maisha ya duniani,
21; Na mnaacha maisha ya Akhera.
22; Zipo nyuso siku hiyo zitao ng´ara,
23; Zinamwangallia Mola wao Mlezi.
24; Na zipo nyuso siku hiyo zitakao kunjana.
25; Zitajua ya kuwa zitafikiwa na livunjalo uti wa mgongo.
26; La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo,
27; Na pakasemwa: Nani wa kumganga?
28; Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki;
29; Na utapo ambatishwa muundi kwa muundi,
30; Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi!
31; Kwa sababu hakusadiki, wala hakusali.
32; Bali alikanusha, na akageuka.
33; Kisha akenda kwa ahali zake kwa matao.
34; Ole wako, ole wako!
35; Kisha Ole wako, ole wako!
36; Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure?
37; Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa?
38; Kisha akawa kidonge cha damu, tena Mwenyezi Mungu akamuumba na akamtengeneza vilivyo.
39; Kisha akamfanya namna mbili, mwanamume na mwanamke.
40; Je! Huyo hakuwa ni Muweza wa kufufua wafu?

Pages ( 75 of 114 ): « Previous1 ... 7374 75 7677 ... 114Next »