Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 72 (Sura 72)
1; Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur´ani ya ajabu!
2; Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi.
3; Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana.
4; Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu.
5; Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu.
6; Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.
7; Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.
8; Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.
9; Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!
10; Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu.
11; Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.
12; Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.
13; Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.
14; Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu.
15; Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.
16; Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli wanywesha maji kwa wingi,
17; Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu.
18; Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
19; Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!
20; Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote.
21; Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni.
22; Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu.
23; Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.
24; Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.
25; Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu.
26; Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake,
27; Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.
28; Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.

Pages ( 72 of 114 ): « Previous1 ... 7071 72 7374 ... 114Next »