Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 76 (Sura 76)
1; Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa.
2; Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona.
3; Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.
4; Hakika Sisi tumewaandalia makafiri minyororo na pingu na Moto mkali.
5; Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyo changanyika na kafuri,
6; Ni chemchem watakao inywa waja wa Mwenyezi Mungu, wakiifanya imiminike kwa wingi.
7; Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana,
8; Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.
9; Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.
10; Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.
11; Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.
12; Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyo subiri.
13; Humo wataegemea juu ya viti vya enzi, hawataona humo jua kali wala baridi kali.
14; Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yataning´inia mpaka chini.
15; Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae,
16; Vya fedha safi kama kiyoo, wamevipima kwa vipimo.
17; Na humo watanyweshwa kinywaji kilicho changanyika na tangawizi.
18; Hiyo ni chemchem iliyo humo inaitwa Salsabil.
19; Na watawazungukia kuwatumikia wavulana wasio pevuka, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizo tawanywa.
20; Na utakapo yaona, utakuwa umeona neema na ufalme mkubwa.
21; Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya at´ilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Mlezi atawanywesha kinywaji safi kabisa.
22; Hakika haya ni malipo yenu; na juhudi zenu zimekubaliwa.
23; Hakika Sisi tumekuteremshia Qur´ani kidogo kidogo.
24; Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt´ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru.
25; Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni;
26; Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu.
27; Kwa hakika watu hawa wanapenda maisha ya kidunia, na wanaiacha nyuma yao siku nzito.
28; Sisi tumewaumba, na tukavitia nguvu viungo vyao. Na tukitaka tutawabadilisha mfano wao wawe badala yao.
29; Hakika haya ni mawaidha; basi anaye taka atashika Njia ya kwenda kwa Mola wake Mlezi.
30; Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ilimu, Mwenye hikima.
31; Humuingiza amtakaye katika rehema yake. Na wenye kudhulumu amewawekea adhabu iliyo chungu.

Pages ( 76 of 114 ): « Previous1 ... 7475 76 7778 ... 114Next »