Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 44 (Sura 44)
1; H´a Mim
2; Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
3; Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.
4; Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
5; Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
6; Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
7; Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini.
8; Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
9; Lakini wao wanacheza katika shaka.
10; Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri,
11; Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
12; Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
13; Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha.
14; Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu.
15; Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile!
16; Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa.
17; Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
18; Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu.
19; Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi.
20; Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe.
21; Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.
22; Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu.
23; Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa.
24; Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa.
25; Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!
26; Na mimea na vyeo vitukufu!
27; Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!
28; Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe.
29; La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula.
30; Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha,
31; Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka.
32; Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe.
33; Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.
34; Hakika hawa wanasema:
35; Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi.
36; Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
37; Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa´ na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.
38; Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo.
39; Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.
40; Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote.
41; Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.
42; Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
43; Hakika Mti wa Zaqqum,
44; Ni chakula cha mwenye dhambi.
45; Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni
46; Kama kutokota kwa maji ya moto.
47; (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu!
48; Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka.
49; Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu!
50; Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka.
51; Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani,
52; Katika mabustani na chemchem,
53; Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana,
54; Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini.
55; Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
56; Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu,
57; Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
58; Basi tumeifanya nyepesi hii Qur´ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.
59; Ngoja tu, na wao wangoje pia.

Pages ( 44 of 114 ): « Previous1 ... 4243 44 4546 ... 114Next »