Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 50 (Sura 50)
1; Qaaf. Naapa kwa Qur´ani tukufu!
2; Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!
3; Ati tukifa na tukawa udongo…? Kurejea huko kuko mbali!
4; Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote.
5; Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.
6; Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.
7; Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.
8; Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.
9; Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.
10; Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,
11; Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.
12; Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi.
13; Na A´di na Firauni na kaumu ya Lut´i.
14; Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa´. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao.
15; Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.
16; Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.
17; Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni.
18; Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.
19; Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.
20; Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.
21; Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.
22; (Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.
23; Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa.
24; Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,
25; Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,
26; Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.
27; Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.
28; (Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu.
29; Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.
30; Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?
31; Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali.
32; Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.
33; Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea-
34; (Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.
35; Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
36; Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia?
37; Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.
38; Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu.
39; Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
40; Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
41; Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.
42; Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.
43; Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
44; Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
45; Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur´ani anaye liogopa onyo.

Pages ( 50 of 114 ): « Previous1 ... 4849 50 5152 ... 114Next »