Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 37 (Sura 37)
1; Naapa kwa wanao jipanga kwa safu.
2; Na kwa wenye kukataza mabaya.
3; Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
4; Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja.
5; Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote.
6; Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.
7; Na kulinda na kila shet´ani a´si.
8; Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.
9; Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.
10; Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng´ara.
11; Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata.
12; Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
13; Na wanapo kumbushwa hawakumbuki.
14; Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara.
15; Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri.
16; Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?
17; Hata baba zetu wa zamani?
18; Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili.
19; Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
20; Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.
21; Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha.
22; Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu –
23; Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!
24; Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa:
25; Mna nini? Mbona hamsaidiani?
26; Bali hii leo, watasalimu amri.
27; Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.
28; Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia.
29; Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini.
30; Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu.
31; Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu.
32; Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
33; Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja.
34; Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu.
35; Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa ´Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna.
36; Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu?
37; Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume.
38; Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.
39; Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
40; Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
41; Hao ndio watakao pata riziki maalumu,
42; Matunda, nao watahishimiwa.
43; Katika Bustani za neema.
44; Wako juu ya viti wamekabiliana.
45; Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem
46; Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao.
47; Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.
48; Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri.
49; Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika.
50; Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe.
51; Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki
52; Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki
53; Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa?
54; Atasema: Je! Nyie mnawaona?
55; Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
56; Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza.
57; Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa.
58; Je! Sisi hatutakufa,
59; Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa.
60; Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa.
61; Kwa mfano wa haya nawatende watendao.
62; Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum?
63; Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu.
64; Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu.
65; Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet´ani.
66; Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.
67; Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.
68; Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
69; Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.
70; Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
71; Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani.
72; Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji.
73; Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa.
74; Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
75; Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
76; Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
77; Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.
78; Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye.
79; Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!
80; Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
81; Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
82; Kisha tukawazamisha wale wengine.
83; Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake,
84; Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima.
85; Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?
86; Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
87; Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote?
88; Kisha akapiga jicho kutazama nyota.
89; Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
90; Nao wakamwacha, wakampa kisogo.
91; Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?
92; Mna nini hata hamsemi?
93; Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia.
94; Basi wakamjia upesi upesi.
95; Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe?
96; Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!
97; Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo!
98; Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.
99; Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa.
100; Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
101; Basi tukambashiria mwana aliye mpole.
102; Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.
103; Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.
104; Tulimwita: Ewe Ibrahim!
105; Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema.
106; Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri.
107; Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu.
108; Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye.
109; Iwe salama kwa Ibrahim!
110; Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
111; Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
112; Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema.
113; Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi.
114; Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni.
115; Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa.
116; Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda.
117; Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha.
118; Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
119; Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye.
120; Iwe salama kwa Musa na Haruni!
121; Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
122; Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini.
123; Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
124; Alipo waambia watu wake: Hamwogopi?
125; Mnamwomba Baa´li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,
126; Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?
127; Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa;
128; Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
129; Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye.
130; Iwe salama kwa Ilyas.
131; Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
132; Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
133; Na hakika Lut´i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume.
134; Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,
135; Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma.
136; Kisha tukawaangamiza wale wengineo.
137; Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,
138; Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?
139; Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.
140; Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni.
141; Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa.
142; Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.
143; Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu,
144; Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa.
145; Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa.
146; Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung´unye.
147; Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi.
148; Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.
149; Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume?
150; Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?
151; Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:
152; Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!
153; Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume?
154; Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?
155; Hamkumbuki?
156; Au mnayo hoja iliyo wazi?
157; Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli.
158; Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa.
159; Subhana ´Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia.
160; Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
161; Basi hakika nyinyi na mnao waabudu
162; Hamwezi kuwapoteza
163; Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni.
164; Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu.
165; Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu.
166; Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa.
167; Na walikuwapo walio kuwa wakisema:
168; Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,
169; Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi.
170; Lakini waliukataa. Basi watakuja jua.
171; Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa.
172; Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa.
173; Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda.
174; Basi waachilie mbali kwa muda.
175; Na watazame, nao wataona.
176; Je! Wanaihimiza adhabu yetu?
177; Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa.
178; Na waache kwa muda.
179; Na tazama, na wao wataona.
180; Subhana Rabbi´l´Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia.
181; Na Salamu juu ya Mitume.
182; Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Pages ( 37 of 114 ): « Previous1 ... 3536 37 3839 ... 114Next »