Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 43 (Sura 43)
1; H´a Mim
2; Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.
3; Hakika Sisi tumeifanya Qur´ani kwa Kiarabu ili mfahamu.
4; Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima.
5; Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri?
6; Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
7; Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
8; Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.
9; Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi,
10; Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka.
11; Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa.
12; Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda.
13; Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe.
14; Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
15; Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri.
16; Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume?
17; Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira.
18; Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana…?
19; Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa!
20; Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
21; Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho?
22; Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao.
23; Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao.
24; Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa.
25; Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha!
26; Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu,
27; Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa.
28; Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee.
29; Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha.
30; Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa.
31; Na walisema: Kwa nini Qur´ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii?
32; Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
33; Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia,
34; Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake,
35; Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu.
36; Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet´ani kuwa ndiye rafiki yake.
37; Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka.
38; Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe!
39; Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu.
40; Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi?
41; Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao.
42; Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao.
43; Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka.
44; Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa.
45; Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah´mani?
46; Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote!
47; Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.
48; Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee.
49; Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
50; Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
51; Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni?
52; Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?
53; Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?
54; Basi aliwachezea watu wake, na wakamt´ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu.
55; Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
56; Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.
57; Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele.
58; Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
59; Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.
60; Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana.
61; Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
62; Wala asikuzuilieni Shet´ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri.
63; Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit´ii mimi.
64; Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
65; Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
66; Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui?
67; Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu.
68; Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
69; Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.
70; Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.
71; Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.
72; Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
73; Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.
74; Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.
75; Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
76; Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.
77; Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
78; Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.
79; Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha.
80; Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong´ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
81; Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu.
82; Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A´rshi, na hayo wanayo msifia.
83; Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa.
84; Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
85; Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.
86; Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
87; Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
88; Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini.
89; Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.

Pages ( 43 of 114 ): « Previous1 ... 4142 43 4445 ... 114Next »