Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 54 (Sura 54)
1; Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!
2; Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea.
3; Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.
4; Na bila ya shaka zimewajia khabari zenye makaripio.
5; Hikima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu!
6; Basi jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha;
7; Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika,
8; Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.
9; Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.
10; Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!
11; Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika.
12; Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa.
13; Na tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba.
14; Ikawa inakwenda kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa.
15; Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka?
16; Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.
17; Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur´ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye kumbuka?
18; Kina A´di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
19; Hakika Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo,
20; Ukiwang´oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng´olewa.
21; Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
22; Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur´ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye kumbuka?
23; Thamudi waliwakanusha Waonyaji.
24; Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!
25; Ni yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!
26; Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.
27; Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili.
28; Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika.
29; Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.
30; Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
31; Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa.
32; Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur´ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye?
33; Kaumu Lut´i nao waliwakadhibisha Waonyaji.
34; Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut´i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.
35; Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru.
36; Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.
37; Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu!
38; Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.
39; Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!
40; Na hakika tumeisahilisha Qur´ani kuikumbuka. Lakini yupo anaye kumbuka?
41; Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.
42; Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza.
43; Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?
44; Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.
45; Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.
46; Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.
47; Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu.
48; Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu!
49; Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
50; Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.
51; Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anaye kumbuka?
52; Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni.
53; Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
54; Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.
55; Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.

Pages ( 54 of 114 ): « Previous1 ... 5253 54 5556 ... 114Next »