Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 25 (Sura 25)
1; Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.
2; Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.
3; Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka.
4; Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo.
5; Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni.
6; Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
7; Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
8; Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
9; Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia.
10; Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari.
11; Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa..
12; Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake.
13; Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe.
14; Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
15; Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
16; Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
17; Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia?
18; Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
19; Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa.
20; Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona.
21; NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!
22; Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali!
23; Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika.
24; Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri.
25; Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi,
26; Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
27; Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume!
28; Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!
29; Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet´ani ni khaini kwa mwanaadamu.
30; Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur´ani ni kihame.
31; Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.
32; Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur´ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
33; Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.
34; Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia.
35; Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.
36; Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa.
37; Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu.
38; Na tuliwaangamiza kina A´di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao.
39; Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.
40; Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.
41; Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume?
42; Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia.
43; Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?
44; Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
45; Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake.
46; Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.
47; Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka.
48; Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.
49; Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba.
50; Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru.
51; Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji.
52; Basi usiwat´ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa.
53; Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.
54; Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.
55; Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.
56; Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
57; Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.
58; Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.
59; Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A´rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye.
60; Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
61; Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng´ara.
62; Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.
63; Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
64; Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.
65; Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.
66; Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya.
67; Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.
68; Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara,
69; Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka.
70; Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
71; Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.
72; Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
73; Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.
74; Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
75; Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.
76; Wadumu humo – kituo na makao mazuri kabisa.
77; Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.

Pages ( 25 of 114 ): « Previous1 ... 2324 25 2627 ... 114Next »