Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 77 (Sura 77)
1; Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole!
2; Na zinazo vuma kwa kasi!
3; Na zikaeneza maeneo yote!
4; Na zinazo farikisha zikatawanya!
5; Na zinazo peleka mawaidha!
6; Kwa kuudhuru au kuonya,
7; Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa!
8; Wakati nyota zitakapo futwa,
9; Na mbingu zitakapo pasuliwa,
10; Na milima itakapo peperushwa,
11; Na Mitume watakapo wekewa wakati wao,
12; Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo?
13; Kwa siku ya kupambanua!
14; Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini?
15; Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha!
16; Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia?
17; Kisha tukawafuatilizia walio fuatia?
18; Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu!
19; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
20; Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa?
21; Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti?
22; Mpaka muda maalumu?
23; Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria.
24; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
25; Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya
26; Walio hai na maiti?
27; Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu?
28; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
29; Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha!
30; Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu!
31; Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako.
32; Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba!
33; Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano!
34; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
35; Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu,
36; Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru.
37; Ole wao siku hiyo hao walio kanusha!
38; Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia.
39; Ikiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi!
40; Ole wao siku hiyo hao walio kanusha!
41; Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem,
42; Na matunda wanayo yapenda,
43; Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.
44; Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema.
45; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
46; Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu!
47; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
48; Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami.
49; Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha!
50; Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?

Pages ( 77 of 114 ): « Previous1 ... 7576 77 7879 ... 114Next »