Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 51 (Sura 51)
1; Naapa kwa pepo zinazo tawanya,
2; Na zinazo beba mizigo,
3; Na zinazo kwenda kwa wepesi.
4; Na zinazo gawanya kwa amri,
5; Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,
6; Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea.
7; Naapa kwa mbingu zenye njia,
8; Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana.
9; Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.
10; Wazushi wameangamizwa.
11; Ambao wameghafilika katika ujinga.
12; Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?
13; Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.
14; Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.
15; Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
16; Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
17; Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.
18; Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
19; Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.
20; Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.
21; Na pia katika nafsi zenu – Je! Hamwoni?
22; Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.
23; Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.
24; Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?
25; Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni.
26; Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.
27; Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?
28; Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.
29; Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!
30; Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua.
31; AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa?
32; Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,
33; Tuwatupie mawe ya udongo,
34; Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.
35; Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini.
36; Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!
37; Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.
38; Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi.
39; Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!
40; Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa.
41; Na katika khabari za A´di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi.
42; Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka.
43; Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu.
44; Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona.
45; Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea.
46; Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu.
47; Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua.
48; Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi!
49; Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.
50; Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
51; Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
52; Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.
53; Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.
54; Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.
55; Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.
56; Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
57; Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.
58; Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.
59; Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize.
60; Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.

Pages ( 51 of 114 ): « Previous1 ... 4950 51 5253 ... 114Next »