Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 70 (Sura 70)
1; Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea,
2; Kwa makafiri – ambayo hapana awezaye kuizuia –
3; Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.
4; Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!
5; Basi subiri kwa subira njema.
6; Hakika wao wanaiona iko mbali,
7; Na Sisi tunaiona iko karibu.
8; Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa.
9; Na milima itakuwa kama sufi.
10; Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake.
11; Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe,
12; Na mkewe, na nduguye,
13; Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu,
14; Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye.
15; La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa,
16; Unao babua ngozi ya kichwa!
17; Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka.
18; Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.
19; Hakika mtu ameumbwa na papara.
20; Inapo mgusa shari hupapatika.
21; Na inapo mgusa kheri huizuilia.
22; Isipo kuwa wanao sali,
23; Ambao wanadumisha Sala zao,
24; Na ambao katika mali yao iko haki maalumu
25; Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba;
26; Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo,
27; Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.
28; Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo.
29; Na ambao wanahifadhi tupu zao.
30; Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi –
31; Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka.
32; Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,
33; Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,
34; Na ambao wanazihifadhi Sala zao.
35; Hao ndio watakao hishimiwa Peponi.
36; Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu?
37; Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!
38; Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema?
39; La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua.
40; Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza
41; Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.
42; Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa,
43; Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo,
44; Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa.

Pages ( 70 of 114 ): « Previous1 ... 6869 70 7172 ... 114Next »