Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 69 (Sura 69)
1; Tukio la haki.
2; Nini hilo Tukio la haki?
3; Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki?
4; Thamudi na A´di waliukadhibisha Msiba unao situsha.
5; Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno.
6; Na ama A´di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika.
7; Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani.
8; Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?
9; Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia.
10; Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu.
11; Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina,
12; Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi.
13; Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu,
14; Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja,
15; Siku hiyo ndio Tukio litatukia.
16; Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.
17; Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
18; Siku hiyo mtahudhurishwa – haitafichika siri yoyote yenu.
19; Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
20; Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.
21; Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza,
22; Katika Bustani ya juu,
23; Matunda yake yakaribu.
24; Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita.
25; Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu!
26; Wala nisingeli jua nini hisabu yangu.
27; Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa.
28; Mali yangu hayakunifaa kitu.
29; Madaraka yangu yamenipotea.
30; (Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!
31; Kisha mtupeni Motoni!
32; Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini!
33; Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu,
34; Wala hahimizi kulisha masikini.
35; Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu,
36; Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.
37; Chakula hicho hawakili ila wakosefu.
38; Basi naapa kwa mnavyo viona,
39; Na msivyo viona,
40; Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima.
41; Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini.
42; Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka.
43; Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
44; Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu,
45; Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia,
46; Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!
47; Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia.
48; Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu.
49; Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha.
50; Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa.
51; Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini.
52; Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu.

Pages ( 69 of 114 ): « Previous1 ... 6768 69 7071 ... 114Next »