Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 79 (Sura 79)
1; Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu,
2; Na kwa wanao toa kwa upole,
3; Na wanao ogelea,
4; Wakishindana mbio,
5; Wakidabiri mambo.
6; Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka,
7; Kifuate cha kufuatia.
8; Siku hiyo nyoyo zitapiga piga,
9; Macho yatainama chini.
10; Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza?
11; Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa?
12; Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara!
13; Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu,
14; Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano!
15; Je! Imekufikia hadithi ya Musa?
16; Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T´uwaa, akamwambia:
17; Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri.
18; Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa?
19; Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha.
20; Basi alimwonyesha Ishara kubwa.
21; Lakini aliikadhibisha na akaasi.
22; Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi.
23; Akakusanya watu akanadi.
24; Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa.
25; Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo.
26; Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa.
27; Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga!
28; Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri.
29; Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake.
30; Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi.
31; Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake,
32; Na milima akaisimamisha,
33; Kwa nafuu yenu na mifugo yenu.
34; Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa,
35; Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya,
36; Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona,
37; Basi ama yule aliye zidi ujeuri,
38; Na akakhiari maisha ya dunia,
39; Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!
40; Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio,
41; Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!
42; Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini?
43; Una nini wewe hata uitaje?
44; Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake.
45; Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu.
46; Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake.

Pages ( 79 of 114 ): « Previous1 ... 7778 79 8081 ... 114Next »