Swahili Quran | Soma Kurani

Chapter 68 (Sura 68)
1; Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo,
2; Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu.
3; Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika.
4; Na hakika wewe una tabia tukufu.
5; Karibu utaona, na wao wataona,
6; Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu.
7; Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.
8; Basi usiwat´ii wanao kadhibisha.
9; Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie.
10; Wala usimt´ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa,
11; Mtapitapi, apitaye akifitini,
12; Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi,
13; Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu.
14; Ati kwa kuwa ana mali na watoto!
15; Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani!
16; Tutamtia kovu juu ya pua yake.
17; Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi.
18; Wala hawakusema: Mungu akipenda!
19; Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala!
20; Likawa kama usiku wa giza.
21; Asubuhi wakaitana.
22; Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna.
23; Basi walikwenda na huku wakinong´onezana,
24; Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni.
25; Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo.
26; Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea!
27; Bali tumenyimwa!
28; Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu?
29; Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu.
30; Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao.
31; Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka!
32; Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
33; Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua!
34; Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi.
35; Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu?
36; Mna nini? Mnahukumu vipi?
37; Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma?
38; Kuwa mtapata humo mnayo yapenda?
39; Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia?
40; Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya?
41; Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli.
42; Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza,
43; Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima –
44; Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua.
45; Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara.
46; Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo?
47; Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika?
48; Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa.
49; Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa.
50; Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema.
51; Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu.
52; Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

Pages ( 68 of 114 ): « Previous1 ... 6667 68 6970 ... 114Next »